Skip to main content
x

Mwanza; Juni 16, 2019: Wakati Tanzania ikiungana na mataifa mengine Ulimwenguni katika kuadhimisha Siku ya Wachangiaji Damu Duniani, Benki ya Exim Tanzania imekabidhiwa tuzo maalum kutoka serikalini ikiwa ni utambuzi wa mchango wa benki hiyo katika kufanikisha suala hilo zima la upatikanaji wa damu salama hapa nchini.

Benki hiyo imekabidhiwa tuzo, hiyo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu katika Maadhimisho hayo yaliyofanyika kitaifa jijini Mwanza, viwanja vya Furahisha mwishoni mwa wiki iliyopita yakiwa na kauli mbiu "Damu Salama Kwa Wote"

Akiipongeza benki hiyo kwa ushiriki wake mkubwa kwenye jitihada za upatikanaji wa damu salama hapa nchini, Waziri Ummy ambaye alikuwa Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo pia alihimiza benki hiyo kuendelea kuwa balozi imara wa damu salama hapa nchini sambamba na kuhamasisha taasisi nyingine na watu binafsi kuunguna na benki hiyo katika kufanikisha mpango huo muhimu.

"Serikali imetenga Sh. bilioni tano katika mwaka wa fedha 2019/20 zitakazotumika kujenga vituo vituo vidogo vya uchangiaji damu salama katika mikoa yote 12 nchini. "Alisema Ummy ambae pia alizindua mashine mpya "full automation" za kupimia maambukizi katika damu na za kupimia makundi ya damu ambazo zimesimikwa kwenye vituo vya kanda sita ikiwamo Dar es Salaam, Mwanza, Tabora, Kilimanjaro, Mtwara na Mbeya.

"Tunataka kumfikia kila mtanzania mwenye mahitaji ya damu salama popote alipo tuhakikishe anapata  damu salama bila kikwazo chochote, WHO inakadiria idadi ya watu 1000 zipatikane chupa 10 za damu. Watanzania tunakadiriwa tupo milioni 55 tunapaswa kupata asilimia moja ya idadi hiyo, hivyo chupa 550,000 zinahitajika kila mwaka kutosheleza mahitaji," alisema.

Akizungumza kuhusiana na tuzo hiyo Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa benki hiyo Bw. Stanley Kafu alisema: "Benki ya Exim tumepokea tuzo na heshima hii kutoka serikalini kwa mikono miwili kwa kuwa ni sehemu ya matokeo chanya ya mkakati wa benki ya Exim ya uwajibikaji kwa jamii unaofahamika kama "Exim Cares". Hivyo tuzo na heshima hii ni kama chachu ya sisi kuendelea kujitoa zaidi katika kufanikisha mpango wa damu salama hapa nchini," alisema.

Kwa mujibu wa Bw. Kafu, mapema mwezi huu benki hiyo kwa kushirikiana na Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS) walianza utekelezaji wa pamoja wa mpango wa uchangiaji wa damu uliohusisha matawi yote ya benki hiyo hapa nchini hususani katika mikoa minane ya Dar es Salaam, Mwanza, Kilimanjaro, Arusha, Mbeya, Tanga, Mtwara na Zanzibar.

"Sisi ni mojawapo ya taasisi ambazo zinaendesha huduma zake katika sehemu kubwa ya nchi hii na huduma yetu inagusa idadi kubwa ya watu. Tunaguswa na jamii tunayoihudumia na tunaamini jamii yenye afya ni muhimu katika kutimiza malengo yetu. Na hiyo ndio sababu tumeelekeza rasilimali zetu pamoja na maeneo ya ofisi zetu kama kambi za kukusanyia damu," alisema Kafu

Benki ya Exim imeendelea kuonyesha uwajibikaji wake katika kusaidia sekta ya afya kupitia mipango mbalimbali na miradi ya kijamii. Katika miaka minane iliyopita benki  imechangia zaidi  ya chupa 1000 za damu katika Benki ya damu Taifa.