Skip to main content
x

Kilimanjaro; Benki ya Exim Tanzania pamoja na Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS) wameingia kwenye makubaliano rasmi ya utekelezaji wa pamoja wa mpango wa uchangiaji wa damu utakaohuisha matawi yote ya benki hiyo hapa nchini.

Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa benki hiyo ya uwajibikaji kwa jamii unaofahamika kama " Exim Cares"

Ushirikiano huo umezinduliwa rasmi leo katika tukio la uchangiaji wa damu lililoandaliwa na benki hiyo kwenye tawi lake lililopo barabara ya Old Moshi katika Manispaa ya Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro ikiwa ni urasimishaji wa jitihada za benki hiyo kwa kipindi cha miaka minane mfululizo katika uchangiaji wa damu hapa nchini.

Akizungumzia mpango huo Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa benki hiyo inayosema " Exim kazini leo kwa ajili ya kesho" na kwamba unalenga kuchangia damu na kutoa elimu ya umuhimu wa kuchangia damu katika mpango wa Taifa.

"Kampeni hii ni sehemu ya uthibitisho kuwa benki ya Exim iko makini kutafuta njia za ubunifu za kuhudumia wateja wake na muhimu zaidi, inajitolea kuhakikisha inashiriki kuleta mabadiliko chanya katika jamii," Alisema Kafu.

Akizungumza kuhusu makubaliano hayona NBTS, Kafu alisema benki hiyo itawezesha mpango na utekelezaji wa uchangiaji damu kwenye kambi nane (8) za uchangiaji damu katika mikoa ya Dar s Salaam, Mwanza, Kilimanjaro, Arusha, Mbeya, Tanga, Mtwara na Zanzibar huku ofisi ya Mpango wa Taifa Damu Salama wakisimamia masuala yote ya kitabibu katika mpango huo.

"Zaidi benki ya Exim kwa kushirikiana wadau wote wa mpango huu wakiwemo Mpango Mpango wa Taifa Damu Salama, Wizara ya Afya na wadau wa habari tutahusika na kuratibu mikakati ya uelimishaji na uhamasishaji wa wananchi ili waweze kujitokeza kwa wingi katika suala hili muhimu kuelekea kilele cha  Maadhimisho ya siku ya kuchangia damu Duniani,"Alisema Kafu

Kwa upande wake Meneja wa NBTS Kanda ya Kaskazini Dk. Edson Mollel alisema ofisi hiyo inahitaji kukusanya chupa (Units) 526,000 za damu ili kukidhi mahitaji ya kila mwaka kwa nchi nzima ambapo kiasi kilichopatikana mwaka jana ilikuwa ni chupa 307,835 sawa na asilimia 58 ya mahitaji.

"Mwaka huu lengo nikukusanya chupa 357,000 za damu na kupitia maadhimisho ya mwaka huu pekee tumejipanga kukusanya chupa 41,920 na ndio maana tunaridhishwa sana wanapojitokeza wadau kama benki ya Exim ili kutuunga mkono...uhitaji wa damu ni mkubwa."

"Hatua hii ni mfano wa kuigwa kwa kuwa benki ya Exim na wafanyakazi wake wanakuwa sehemu ya jamii wanayoihudumia kwa ukaribu zaidi na pia wanathibitisha rasmi mioyo yao ya kujitolea kwa hali na mali kwa jamii wanayoihudumia," Alisema.

Benki ya Exim imeendelea kuonyesha uwajibikaji wake katika kusaidia sekta ya afya kupitia mipango mbalimbali na miradi ya kijamii. Katika miaka minane iliyopita benki imechangia zaidi ya lita 100 za damu katika Benki ya damu Taifa.